Рет қаралды 3,001
Baada ya mkutano mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kumalizika kwa kupata Mkuu wa kanisa hilo mpya, Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza ameibuka na mambo matatu.
Askofu Bagonza ameeleza mambo hayo baada ya juzi usiku Alhamisi Agosti 24,2023 kuhitimishwa kwa uchaguzi ambapo Askofu Alex Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani kuibuka mshindi wa Mkuu wa KKKT akichukua nafasi iliyoachwa na Askofu Fredrick Shoo aliyemaliza muda wake wa uongozi.
Askofu huyo ametumia kurasa zake za kijamii, kuandika ujumbe wenye mambo matatu ya kufikirisha akiupa kichwa cha habari 'hatugombei, tunagombezwa.'
Ujumbe huo wa Askofu Bagonza unasema:
Wapendwa wangu, nimejizuia sana kuandika au kusema chochote. Lakini mmenisonga sana, nami nimo safarini. Kwa kuwa sijui kama nitafika niendako (Vienna) kabla hamjakata tamaa na kuzimia, naomba msome kwa furaha mambo haya matatu:
1. Tumetazamwa na dunia nzima kwa siku nne. Mmoja aliyeona na alikuwa mgeni akaniuliza: “Hivi nyie wenzetu Wachungaji na Maaskofu mmeishagundua mbingu haipo mkafanya iwe siri yenu tu?” Akaongeza, “kama mbingu ipo kwa nini mfanyiane haya mabaya hadharani?
2. Nilizoezwa kuamini kuwa watu wanakataliwa kwa sababu ya ubaya wao na wengine hupendwa kwa sababu ya uzuri wao. Sasa nimeamini wapo wanaoweza kukataliwa kwa uzuri na wakapendwa kwa ubaya wao. Cha msingi, ubaya hauwezi kukaa kwa amani na wema. Tumefundishwa:
Katika Agano la Kale, kichafu kikigusana na kitakatifu, kile kitakatifu kinaharibika.
Katika Agano Jipya, kichafu kikigusana na kitakatifu, kile kichafu kinatakasika. TKKK ni ya Agano Jipya au la Kale?
3. Watu wakatili na waovu hujiandaa kupiga na kuangamiza wabaya wao wakati wote. Watu wema hutafuta kuushinda ubaya kwa wema.
Hutokea wakati, wapigaji wakapiga na kufurahi kuwa wamepiga. Wakitulia hugundua kuwa kumbe wamepigwa sana. Kutosamehe ni sawa na kunywa sumu ukitegemea afe adui yako. Sumu uliyokumywa bila kukusudia inaua vibaya.
Humu kibandani kwetu huwa hatugombei bali tunagombezwa na kuzodolewa.
Unione nitakapokuona.